Dodoma FM

Ukosefu wa umeme wakwamisha maendeleo ya vitongoji Mbelezungu

17 November 2026, 16:21

Picha ni mitambo inayotumika katika usambazaji wa nishati ya umeme, Picha na Mwananchi.

Wananchi wa kijiji cha Mbelezungu, Mkoani Dodoma wanatarajia kuwa hatua za serikali kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO zitaongeza kasi ya kusambaza umeme katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa, ili kuwawezesha kupata huduma hiyo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Na Victor Chigwada.

Wakazi wa Kijiji cha Mbelezungu, Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, wameiomba serikali kuharakisha usambazaji wa huduma ya umeme katika vitongoji vya kijiji hicho, wakieleza kuwa ukosefu wa nishati hiyo unawanyima fursa mbalimbali za kijamii na kiuchumi zinazotegemea umeme.

Wakizungumza na Taswira ya Habari, wananchi hao wamesema baadhi ya shughuli za maendeleo zinakwama kutokana na kutofikiwa na huduma hiyo, huku wakieleza kuwa upatikanaji wa umeme utasaidia kurahisisha shughuli za kila siku na kufungua fursa mpya za kiuchumi katika maeneo yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbelezungu, George Isaya, amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo, akieleza kuwa baadhi ya vitongoji bado havijafikiwa na huduma ya umeme, hali inayozikosesha baadhi ya taasisi muhimu, ikiwemo shule na taasisi za dini, fursa ya kutumia nishati hiyo katika shughuli zao.

Amesema licha ya vipimo vya awali vya usambazaji wa umeme kufanyika katika Vitongoji vya Mbelezungu B na Manzilanzi A, huduma hiyo bado haijawafikia wananchi wote, huku baadhi ya maeneo yakiwa bado hayajafanyiwa tathmini ya awali kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.

Ripoti ya Victor Chigwada.