Dodoma FM

Serikali yaendelea kusisitiza huduma za usafi wa mazingira

2 July 2026, 17:16

Picha ni ufunguzi wa Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafi wa Mazingira (2nd National Sanitation Forum) lililofanyika jijini Dodoma.Picha na Anwary Shaban.

Jukwaa hilo la siku mbili linaendelea hadi Julai 3, 2026, likiwakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu, wadau wa maendeleo na sekta binafsi kujadili namna ya kuimarisha huduma za usafi wa mazingira zinazowajumuisha watu wote kwa ajili ya maendeleo endelevu nchini.

Na Anwary Shaban.

Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa huduma za usafi wa mazingira zinazomfikia kila mwananchi bila ubaguzi, ikieleza kuwa hatua hiyo ni msingi wa kulinda afya za wananchi na kufanikisha maendeleo endelevu nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 2, 2026, wakati wa ufunguzi wa Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafi wa Mazingira (2nd National Sanitation Forum) lililofanyika jijini Dodoma, likiwa na kaulimbiu isemayo “Huduma za Usafi wa Mazingira Zinazojumuisha Watu Wote kwa Ajili ya Maendeleo Endelevu.”

Akifungua jukwaa hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu wa Watu Wenye Ulemavu, Mheshimiwa Profesa Palamagamba  Kabudi, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma bora za usafi wa mazingira zinapatikana kwa wananchi wote, wakiwemo watu wenye ulemavu na makundi mengine yenye mahitaji maalumu, ili kuboresha afya na ustawi wa jamii.

Sauti ya Profesa Palamagamba  Kabudi.
Picha ni ufunguzi wa Jukwaa la Pili la Kitaifa la Usafi wa Mazingira (2nd National Sanitation Forum) lililofanyika jijini Dodoma.Picha na Anwary Shaban.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Stanley Mahembe, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, amesema mamlaka hiyo itaendelea kusimamia na kuimarisha huduma za maji na usafi wa mazingira kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma salama, zenye ubora na zinazokidhi viwango.

Sauti ya Stanley Mahembe,

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Alhaj Jabir Shekimweri, amesema Mkoa wa Dodoma utaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote wa sekta ya usafi wa mazingira ili kuhakikisha kampeni na programu mbalimbali za usafi zinafanikiwa na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Sauti ya Alhaj Jabir Shekimweri.