Dodoma FM

Serikali kupitia JKT kuwafundisha stadi za kazi watoto waishio katika makao ya watoto

6 July 2023, 5:22 pm

Brigedia Jenerali Mabena amesema dhumuni la ujio wao katika makao hayo ya Taifa ya watoto Kikombo ni kutaka watoto kujengewa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji kwenye jamii kupitia shughuli mbalimbali. Picha na JKT.

Jeshi la Kujenga Taifa JKT limekabidhi msaada wa mchele, sukari, mafuta ya kupikia, chumvi na unga wa ugali unaozalishwa na vijana walioko kwenye kambi mbalimbali za JKT nchini.

Na Mariam Matundu.

Serikali kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) imeandaa mkakati wa kuwajengea uwezo wa kujitegemea watoto waishio katika makao ya watoto nchini kwa kuwafundisha stadi za kazi zitakazowawezesha kufanya uzalishaji ili kuondokana na idadi ya vijana tegemezi wanaoishia kujihusisha na vitendo viovu.

Hayo yamebainishwa na mkuu wa utawala kutoka Jeshi la Kujenga Taifa Brigedia Jenerali Hassan Mabena, alipotembelea Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo jijini Dodoma Julai 5, 2023 kwa lengo la kukabidhi msaada wa chakula kwa watoto waishio kwenye makao hayo.

Brigedia Jenerali Mabena amesema dhumuni la ujio wao katika makao hayo ya Taifa ya Watoto Kikombo ni kutaka watoto kujengewa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji kwenye jamii kupitia shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo ili kuondokana na wimbi la watoto na vijana waliojaa mtaani bila kazi yoyote.

Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wenye lengo la kuwainua na kuwatengenezea mazingira bora watoto . Picha na JKT.

Akitoa maelezo kuhusu kituo hicho Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Tullo Masanja amesema Makao hayo yenye uwezo wa kuhudumia watoto 150, yana eneo kubwa la kuwezesha watoto hao kufanya elimu kwa vitendo ikiwemo eneo la shanba na karakana za ufundi.

Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wenye lengo la kuwainua na kuwatengenezea mazingira bora watoto waishio kwenye makao mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha kulelea watoto Kikombo, Johnas Tarimo ameshukuru na kupongeza jitihada za Jeshi la Kujenga Taifa kusaidiana na Wizara katika kutoa stadi za kazi kwa watoto waliopo kwenye Makazi hayo kwani itakua chachu wa watoto hao kujifunza zaidi kwa vitendo.