Dodoma FM

Nagulo Bahi wanafunzi kuanza masomo rasmi

7 April 2021, 9:03 am

Na ; Suleiman Kodima.

Wananchi wa kijiji cha Nagulo Bahi kata ya Bahi wameupongeza Uongozi wa kata hiyo kwa hatua ya kukamilisha Ujenzi wa Sekondari na hatimaye wanafunzi kuanza Masomo Rasmi.

Wakizungumza na Taswira ya Habari wananchi hao wamesema kuwa juhudi zilizofanywa na uongozi wa kijiji pamoja na Kata ni Ishara ya kuondoa na kupunguza changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza  kwa baadhi ya wanafunzi kushindwa kumaliza Elimu yao ya Sekondari .

Wamesema kutokana na sekondari ya Nagulo bahi kuanza Rasmi na wanafunzi kuanza masomo ni muda kwa wazazi na walezi kuhimizana juu ya umuhimu wa watoto wote kusoma bila kuwa na sababu nyingine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Nagulo Bw.Ashery Ojuku amesema wamekwisha kukamilisha ujenzi wa madarasa mawili pamoja na Ofisi moja ya walimu  hivyo ni muda wa wazazi kutoa nafasi kwa watoto kupata haki yao ya Elimu na kuacha tabia ya kuwatumia  katika shughuli za kiuchumi .

Naye Diwani wa Kata ya Bahi Augustino Ndunu amesema kuwa wamemaliza lengo namba moja la Ujenzi wa Madarasa Mawili sasa wanageukia Lengo namba mbili la kuanza Ujenzi mwingine ikiwa ni sehemu ya kuendeleza Sekondari hiyo.

Huu ni Mwendelezo wa Miradi ambayo wananchi wamekuwa wakiendelea kushirikiana na Serikali katika kutambua Umuhimu wa kusogeza huduma za Msingi karibu na Jamii.