Lugha ya kiswahili ni fursa ya kiuchumi duniani
7 July 2023, 2:58 pm
Mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu zimetakiwa kuhakikisha kuwa wanaandaa na kuratibu mipango ya kutafuta nafasi za kufundisha lugha ya Kiswahili katika Nchi mbalimbali ili Watanzania waweze kwenda kutumia fursa hizo.
Na Mindi Joseph.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuzungumza na kusoma lugha ya Kiswahili kwa kuwa lugha hiyo ni fursa ya kiuchumi Duniani.
Ametoa wito huo wakati akifungua maadhimisho ya Siku ya Kiswahili duniani.
Amesema kuwa Watanzania wananafasi ya kuwa walimu kwenye nchi mbalimbali ambazo zimeingiza katika mitaala yao somo la Kiswahili.
Naye, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Pindi Chana amesema kuwa lugha ya kiswahili imeendelea kukua kwa kasi duniani ambapo takwimu zinaonesha kuwa takribani watu milioni 500 wanatumia lugha hiyo.