Dodoma FM

Tanzania na Korea zatiliana saini mkopo wa Bilioni 684.6 kusaidia miradi mbalimbali

8 December 2020, 12:48 pm

Pichani kushoto ni Katibu mkuu Wizara ya Fedha na Miopango Bw.Dotto James na Kulia ni Balozi wa Korea Kusini nchini Cho Tae-Ick

Na Alfred Bulahya,

Dodoma.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini Mkataba na Serikali ya Jamhuri ya Korea wenye thamani ya dola za Marekani milioni 300, sawa na shilingi bilioni 684.6 za Tanzania kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali nchini.

Hafla hiyo ya utiaji saini imefanyika leo Jijini Dodoma na kuhusisha viongozi mbalimbali wa pande zote mbili ambapo mikopo hiyo yenye masharti nafuu ni kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi (EDCF).
Akizungumza katika hafla hiyo katibu mkuu wizara ya fedha na mipango bw, Doto James, amesema mkopo huo utakwenda kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo Ujenzi wa Vituo viwili vya kupoozea Umeme katika njia ya kusafirisha umeme ya Kigoma – Nyakanazi, na Kusaidia bajeti kuu ya Serikali, Ili kuziba pengo la kibajeti lililotokana na madhara ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu inayosababishwa na Virusi vya Korona (COVID – 19).

Mingine ni Uboreshaji wa Huduma za Majitaka jijini Dodoma, ili kuboresha mfumo wa Majitaka Jijini Dodoma kwa kujenga mtambo wa kutibu majitaka na kupanua wigo wa mabomba ya majitaka ili kuongeza idadi ya watu wanaoweza kupata huduma za majitaka, na kupunguza uchafuzi wa mzingira chini na juu ya ardhi.

Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Cho Tae-Ick, amesema moja ya njia za kupata maendeleo ni kupitia mikopo hivyo kama serikali ya korea itaendelea kuja kuwekeza nchini Tanzania kupitia miradi ya kimkakati na kutoa mikopo zaidi ili kuiwezesha nchini kuendelea kiuchumi.
Akizungumza kwa niaba ya watekelezaji wa miradi hiyo Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, amesema ni jukumu lao kuhakikisha wanaisimamia kikamilifu ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.