Dodoma FM

Tume ya haki za binadamu kushirikiana na LHCR

18 August 2021, 1:19 pm

Na; Alfred Bulahya.

Tume ya haki za Binadamu na Utawala Bora imesaini mkataba wa makubaliano mengine ya kushirikiana kufanya kazi na kituo Cha sheria na haki za Binadamu LHCR Kwa ajili ya kulinda, kutetea na kustawisha haki za makundi maalumu wakiwemo wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.

Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu katibu mtendaji wa Tume hiyo, Nobar Bassey wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika Ofisi za tume hiyo zilizopo Jijini Dodoma.

Nobar amesema mashirikiano kati ya tume na kituo Cha sheria na haki za Binadamu ni wamanufaa kwa kuwa LHRC wamefika katika maeneo mengi ya Nchi hivyo itakuwa ni rahisi kuwafikia wananchi wengi Kwa muda mchache.

Aidha ameongeza kuwa kwakushirikiana na kituo hicho watatoa elimu Kwa viongozi ngazi ya Wilaya kuhusu masuala ya haki za Binadamu na Utawala Bora na kujadili kuhusiana na uanzishwaji wa club za nidhamu na Utawala Bora kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Kwa upande wake mkuu wa Ofisi za kituo Cha sheria na haki za Binadamu Dodoma, William Mtwazi amesema kama kituo wamesaini mkataba huo kwa malengo ya kuifikia jamii ya Nchi nzima kwa kutoa Msaada katika masuala ya haki za Binadamu na wamenuia kufanya kazi Kwa karibu na wadau muhimu kama Serikali.