Dodoma FM

Viongozi wa dini na waumini wapigwa msasa

6 February 2023, 3:50 pm

Waumini wakipatiwa elimu juu ya mapambano dhidi ya ukatili wa watoto , utoro kwa wanafunzi pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya . Picha na Benard Mgaya.

Rai imetolewa kwa viongozi wote wa dini katika sehemu za Ibada kukemea utoro wa wanafunzi, ukatili  pamoja na matumizi ya dawa za kulevya ili kuwa na kizazi chenye maadili na hofu ya Mungu.

Na Benard Magawa

Jeshi la Polisi wilaya ya Bahi mkoani Dodoma limetoa elimu kwa viongozi wa dini na waumini kuhusiana na ukatili wa watoto, utoro wa wanafunzi mashuleni pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya ili kuwa na jamii yenye amani na utulivu.

Elimu hiyo imetolewa na Askari kata wa kata ya Bahi Inspekta Tiimanywa alipokuwa akizungumza na viongozi wa kanisa katoliki Parokia ya bahi kupitia mkutano wa kawaida wa viongozi uliofanyika February 4,2023 Parokiani hapo ukiwashirikisha viongozi wa Parokia nzima.

Amesema nivema kujiridhisha kwa kina juu ya  tabia za walezi wanaowakabidhi kulea watoto wao kanisani kama vile watoto wa Sunday schools na vipindi vingine vya watoto kwani watoto wanaweza kuharibiwa na walezi haohao wanaowaamini.

“ Kwa sasa vitendo vya ulawiti vimekithiri kwa baadhi ya walezi wanaopewa thamana ya kulea watoto, hivyo tusipokuwa makini tutajikuta tuna viongozi mashoga, watoto mashoga na hata viongozi mashoga, niombe kila mzazi kuhakikisha anamlinda mtoto wake dhidi ya ukatili wa kila aina.” Alisema Tiimanywa.

Inspecta Timanywa.

Tiimanywa amesema kutowapa mahitaji ya shule na kuwasimamia watoto  kupata elimu ni ukatili unaofanywa na wazazi kwa kuwanyima haki yao ya msingi na kuwaasa wazazi kuwajibika vema kuhakikisha watoto wao wanapata elimu kwani ni haki yao ya msingi huku akikemea vikali suala la utoro wa wanafunzi mashuleni.

Akizungumzia kuhusu matumizi ya madawa ya kulevya Inspekta Tiimanywa amewaasa viongozi na wananchi kwa ujumla kutoa faarifa fiche juu ya watu wanaosambaza madawa hayo wakamatwe ili kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya na kuokoa vijana wanaoteketea na madawa hayo.

“ Nafikiri  platform za kukemea utumiaji wa madawa ya kulevya kanisa wanazo, tunahitaji Bahi safi ambayo ina watu wasiotumia madawa ya kulevya katika maeneo yetu kwani yanaharibu vijana wengi ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.” Alisema Tiimanywa

Inspekta Timanywa.