Dodoma FM

Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kuvaa miwani ya urembo bila kufanya uchunguzi wa macho

25 October 2021, 10:48 am

Na; Alfred Bulahya.

Jamii imetakiwa kuacha tabia ya kuvaa miwani ya urembo bila kufanya uchunguzi wa miwani hiyo ili kuepusha kupata magonjwa yasiyo ya lazima.

Wito huo umetolewa na mtaalamu wa afya kutoka hospital ya rufaa ya mkoa wa Dodoma Dkt Msigaro Leah Erasto, wakati akizungumza na taswira ya habari .

Amesema utumiaji wa miwani bila kupima ni jambo ambalo husababisha baadhi ya watu kupata magonjwa ya macho kama uoni hafifu, presha ya macho na mtoto wa jicho.

Pamoja na hayo amesema ni vyema jamii ikajenga desturi ya kupima macho kila baada ya miezi sita hadi mwaka mmoja hali ambayo itasaidia kutambua afya zao na kuchukua hatua iwapo mtu atabaini kuwepo kwa changamoto kwenye macho yake.

Hata hivyo amedai kuwa kwa sasa wanaendelea na kampeni ya kitaifa na kimataifa ya kutoa huduma na elimu kwa jamii kupitia Nyanja mbalimbali kama vyombo vya habari, lengo ni kuielimisha jamii ichukue hatua za kupima na kupata huduma.

Baaadhi ya wananchi jijini Dodoma wamesema kuwa ni muhimu sasa serikali ikaweka mkazo katika kutoa elimu hiyo kwa kujikita hasa kwenye maeneo ya vijijini na sio kuishia mjini pekee ili kuongeza hamasa kwa jamii kujitokeza kupima na kupata huduma za macho.

Hadi sasa idadi ya wagonjwa wa macho duniani inaendelea kuongzeka kutokana na sababu mbalimbali huku takwimu kutoka kwa watalaamu wa afya zikieleza kuwa takribani watu milioni 2.4 wanamatatizo ya macho nchini Tanzania.