Dodoma FM

TCDC yazindua kampeni ya upandaji miti kwa vyama vya ushirika

11 January 2024, 7:20 pm

Picha ni Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Benson Ndiege akiongea na vyombo vya habari baada ya uzinduzi huo. Picha na Fred Cheti.

Tume hiyo inasimamia vyama vya ushirika nchini na vilivyopo hadi sasa ni 7400 na zoezi hilo litafanyika nchi nzima.

Na Fred Cheti.

Kampeni ya upandaji miti kwa vyama vya ushirika imezinduliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia kukabilina na mabadiliko ya tabianchi.

Uzinduzi huo umefanywa leo Januari 11,2024 na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Benson Ndiege, baada ya kupanda miti katika shule ya Msingi Uhuru jijini Dodoma.

Mrajisi huyo, ametoa wito  kwa  vyama vya Ushirika ambavyo vina mashamba viendelee kupanda miti kwenye taasisi za umma, kwani shughuli za ushirika ni shughuli za kiuchumi.

Picha ni wadau wa vyama vya ushirika wakiwa katika uzinduzi huo. Picha na Fred Cheti.

Kwa upande wake Mtendaji wa SACCOS ya Mamlaka ya kusimamia ununuzi wa umma Bi. Janeth Kalinga amesema kuwa wanaahidi kutekeleza mkakati huo wa upandaji miti katika chama chake cha akiba na mikopo ili kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo.

Naye, Ofisa Misitu daraja la pili kutoka Wakala wa Misitu (TFS), Leonard Bilomo,ameipongeza Tume hiyo kwa juhudi hizo na kusisitiza kusimamia miti hiyo inayopandwa itunzwe na kukua.