Michezo ni sehemu muhimu katika ukuaji wa mtoto
26 June 2026, 15:41

Hata hivyo, baadhi yao wameonya kuwa michezo inaweza kuwa na hatari iwapo watoto watacheza bila uangalizi wa watu wazima.
Na Daniel Njau.
Michezo imeendelea kutajwa kuwa sehemu muhimu katika ukuaji wa watoto, huku wananchi wakisema huwasaidia kuwa wachangamfu, kujifunza kushirikiana na wenzao pamoja na kuimarisha afya ya mwili na akili.
Wananchi waliozungumza wamesema michezo huwajengea watoto uwezo wa kushirikiana, kuwasiliana na wenzao na kuwaondolea msongo wa mawazo unaotokana na shughuli za shule na maisha ya kila siku. Wameeleza kuwa muda wa kucheza ni muhimu kwa maendeleo ya mtoto na unapaswa kupewa kipaumbele.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza kuwa si michezo yote iliyo salama kwa watoto, hasa inapofanyika bila uwepo wa wazazi au walezi. Wamesema uangalizi wa karibu unahitajika ili kuzuia ajali na kuhakikisha watoto wanacheza katika mazingira salama na yanayofaa.
Kwa upande wake, mlezi katika kituo cha world vision cha Watoto amesema michezo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa watoto kimwili, kiakili na kijamii.
Amehimiza wazazi na walezi kuwapa watoto muda wa kucheza na kujumuika na wenzao baada ya kumaliza shughuli za nyumbani na masomo, akieleza kuwa hatua hiyo huchangia kukuza vipaji, kuimarisha afya na kuwajengea watoto kujiamini.