Dodoma FM

Wananchi Chiwoni wafanya harambee ujenzi wa shule shikizi

20 July 2026, 17:25

Picha ni wakazi wa kijiji cha Chiwona kata ya Makang’wa wilayani Chamwino wakiwa katika harambee hiyo.Picha na Anwary Shaban.

Juhudi hizi za wananchi zinaonesha namna ushirikiano kati ya jamii, viongozi na wadau unavyoweza kuwa chachu ya maendeleo ya elimu. Kukamilika kwa shule hiyo kunatarajiwa kupunguza adha ya wanafunzi kutembea umbali mrefu na kuongeza fursa ya watoto wengi kupata elimu katika mazingira bora.

Na Anwary Shaban.

Wakazi wa Kijiji cha Chiwona kata ya Makang’wa wilayani Chamwino wamefanya harambee ya kuchangia ujenzi wa shule shikizi katika kitongoji cha Chiponzi ili kuwapunguzia wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shuleni.

Taswira Habari imefika katika kijiji hicho na kushuhudia wananchi wakishiriki shughuli mbalimbali za ujenzi kwa nguvu zao wenyewe pamoja na kuchangia fedha na vifaa kwa ajili ya kufanikisha ujenzi huo wa shule shikizi.

Akizungumza katika mkutano huo wa uchangishaji , Diwani wa Kata ya Makang’wa,Bi. Dina Menda, amesema anaendelea kutekeleza ahadi yake ya kusaidia ujenzi wa shule hiyo, ambapo kati ya mifuko 50 ya saruji aliyoahidi tayari amekabidhi mifuko 30, huku kati ya shilingi laki nne alizoahidi ameshatoa shilingi laki tatu.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wananchi wa Chiwona waishio Jijini Dar es Salaam, Tito Chahonza, amesema umoja huo wenye wanachama zaidi ya 70 ulianzishwa kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kijiji, hususan sekta ya elimu.

Amesema kupitia harambee waliyoifanya wamefanikiwa kukusanya shilingi milioni tatu, laki tisa, elfu kumi na tisa na mia tano kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa shule hiyo shikizi.

Picha ni wakazi wa kijiji cha Chiwona kata ya Makang’wa wilayani Chamwino wakiwa katika harambee hiyo.Picha na Anwary Shaban.

Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Chiwona wamesema changamoto ya umbali mrefu wa kufuata shule ndiyo iliyowasukuma kuanzisha ujenzi wa shule hiyo shikizi.

Wameeleza kuwa wakati wa msimu wa mvua wanafunzi wengi hushindwa kwenda shule kutokana na hatari ya kuvuka maeneo yenye maji, jambo linalochangia kudumaa kwa elimu Pia wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kuwaunga mkono ili kukamilisha ujenzi wa shule hiyo kwa wakati.

Sauti ya habari