Wajawazito waonywa matumizi holela ya dawa
1 September 2026, 16:41

Daktari Benny Kimaro amesisitiza umuhimu wa wanawake wajawazito kutotumia dawa kwa mazoea au kufuata ushauri wa watu wasio wataalamu wa afya, bali kufika katika vituo vya afya wanapokuwa na tatizo na kupata ushauri kuhusu dawa inayofaa, kipimo na muda wa matumizi. Hata hivyo, wanawake wajawazito wanaaswa kuacha kutumia dawa kwa mazoea na badala yake kupata huduma za kitaalamu na kufata ushauri wa wataalamu wa afya ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza.
Na: Elizabeth Mwinuka.
Matumizi ya dawa bila ushauri wa mtaalamu wa afya wakati wa ujauzito yameelezwa kuwa miongoni mwa mambo yanayoweza kuhatarisha afya ya mama na mtoto, hasa pale dawa zinapotumiwa bila kufahamu aina, kipimo na usalama wake katika kipindi cha ujauzito.
Baadhi ya wananchi jijini Dodoma wameeleza sababu zinazowafanya baadhi ya wajawazito kutumia dawa holela kuwa ni pamoja na kujiona wanafahamu dawa kutokana na matumizi ya awali, kushauriwa na ndugu au marafiki, kukosa muda wa kwenda hospitali pamoja na kutaka kupata nafuu ya haraka wanapopata changamoto za kiafya.
Akizungumzia matumizi ya dawa wakati wa ujauzito, Dkt Benny Kimaro Daktari wa magonjwa ya wanawake na uzazi amesema baadhi ya dawa zinaweza kuwa na madhara kwa mama na mtoto iwapo zitatumiwa bila kufanyiwa tathmini na kupewa maelekezo na mtaalamu wa afya.