Bilioni 7.3 yawekezwa katika kifaa cha kisasa cha kutibu saratani
19 August 2026, 16:45

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia za kisasa, huku ikilenga kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
Na Anwary Shaban.
Serikali imewekeza kiasi cha shilingi bilioni 7.3 katika kifaa cha kisasa cha kutibu saratani, ambacho kina uwezo wa kulenga chembe zilizoathirika na ugonjwa huo bila kuathiri chembechembe nyingine zilizo salama.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo, akiwa katika ofisi za Idara ya Habari Maelezo, ambapo amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha huduma za matibabu ya saratani nchini.
Aidha, Dkt. Msemo amesema Taasisi ya Saratani Ocean Road imenunua mashine nyingine mbili za mionzi ambazo zinatarajiwa kuanza kutumika mwezi Oktoba mwaka huu, hatua itakayosaidia kuongeza uwezo wa kutoa huduma na kupunguza muda ambao wagonjwa hutumia kusubiri matibabu.
Sambamba na hilo, amesema Serikali pia imewekeza katika kifaa cha PET Scan chenye thamani ya kati ya shilingi bilioni 19 hadi 20, ambacho kina uwezo wa kusaidia kubaini na kufuatilia saratani katika hatua za awali, hivyo kuwawezesha wagonjwa kupata matibabu mapema na kuongeza nafasi ya kupona.