Dodoma FM

Je, ni lazima kutumia mamilioni ya shilingi kununua jeneza?

9 September 2026, 17:18

Majeneza hayo hutofautiana kwa bei kulingana na aina ya mbao, ubora wake, mapambo pamoja na muundo wake. Picha na Mathias Mgale.

Wataalamu wa masuala ya kifedha na kijamii wanashauri familia kupanga mapema gharama za mazishi na kufanya maamuzi yanayolingana na uwezo wao wa kifedha ili kuepuka kuacha mzigo wa madeni baada ya msiba.

Na Mathias Mgale.

Taratibu za mazishi katika jamii za Watanzania hutofautiana kulingana na kabila, dini, eneo, na mila za familia hakuna utaratibu mmoja unaowakilisha Watanzania wote. Kwa mfano, mila za Wachagga, Wasukuma, Wazaramo, Wahaya, Wamakonde na jamii nyingine zinaweza kutofautiana sana, na pia taratibu za mazishi ya Kiislamu na Kikristo zina tofauti kubwa.

Baadhi ya familia hutumia fedha nyingi kununua majeneza ya gharama kubwa kwa ajili ya kuwahifadhi na kuwaaga wapendwa wao kwa heshima wakati wa mazishi.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanaona gharama hizo kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya mazishi, huku wengine wakiamini kuwa ni matumizi yanayoweza kuepukika.

Akizungumzia hali hiyo, mtaalamu wa masuala ya mazishi na muuza majeneza, Yassini Sanyeo, anasema mtazamo wa jamii kuhusu heshima kwa marehemu ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya watu kuchagua majeneza ya gharama kubwa.

Anasema katika baadhi ya familia, jeneza la gharama kubwa huonekana kama ishara ya upendo, heshima na kuthamini maisha ya marehemu, jambo ambalo wakati mwingine huifanya familia kutumia fedha nyingi zaidi ya uwezo wao.

Sauti na Mathias Mgale.