Dodoma FM

Wananchi watakiwa kuzingatia lishe ili kujenga jamii yenye afya

25 June 2026, 17:06

Lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa lishe bora.Picha na Anwary Shaban.

Maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe katika Kijiji cha Gawaye yamekuwa jukwaa muhimu la kuwajengea wananchi uelewa kuhusu umuhimu wa lishe bora, kinga dhidi ya magonjwa na matumizi sahihi ya huduma za afya, hatua inayotarajiwa kuimarisha ustawi wa jamii na kupunguza changamoto za afya katika eneo hilo.

Na Mariam Kasawa.

Wananchi wa Kijiji cha Gawaye, Kata ya Chihanga jijini Dodoma wamehimizwa kuendelea kuzingatia masuala ya afya na lishe bora ili kujenga jamii yenye afya njema na kupunguza tatizo la utapiamlo, hususan kwa watoto, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha.

Wito huo umetolewa katika maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe yaliyofanyika katika Kituo cha Kutolea Huduma cha Gawaye ambapo Shirika la Action for Community Care (AFCC) kwa kushirikiana na wataalamu wa afya na viongozi wa Serikali za Mitaa, limeendesha shughuli mbalimbali za utoaji elimu ya afya na lishe kwa wananchi wa Kijiji cha Gawaye, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha afya za jamii.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Meneja Mradi wa Shirika la Action for Community Care Dodoma, Margret Mukama, amesema lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa lishe bora, huduma za afya na matumizi sahihi ya huduma zinazotolewa katika vituo vya afya.

Naye Afisa Lishe, Frida Mollel, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia mlo kamili unaojumuisha makundi yote ya vyakula ili kukabiliana na changamoto za utapiamlo na magonjwa yanayotokana na lishe duni.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo wa Kata ya Chihanga, Hamisi Mgogolo, amesema ushirikiano kati ya wananchi, wataalamu wa afya na wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora na maendeleo endelevu.

Baadhi ya wananchi walioshiriki maadhimisho hayo wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kubadili baadhi ya tabia zisizofaa na kuimarisha afya za familia zao.