Serikali yahimiza uwekezaji katika Tafiti na ubunifu nchini
19 June 2026, 18:33

Prof. Mkenda ametoa wito kwa watafiti, wahadhiri na wadau wa elimu kutumia fursa hiyo kuwasilisha tafiti zenye tija kwa jamii, akisisitiza kuwa maendeleo ya Tanzania yanategemea kwa kiasi kikubwa matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu katika kutatua changamoto za wananchi.
Na Anwary Shaban.
Serikali imeendelea kuhimiza uwekezaji katika tafiti na bunifu kama njia ya kuharakisha maendeleo ya taifa, hususan katika sekta za sayansi, hisabati, afya na teknolojia ya mawasiliano.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa utoaji wa Taarifa za Tuzo za Umahiri wa Utafiti kwa wahadhiri na watafiti kutoka taasisi za elimu ya juu za serikali na zisizo za serikali, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayochochea tafiti zenye majibu ya changamoto zinazoikabili jamii.
Amesema tafiti zina mchango mkubwa katika kuongeza maarifa, kuibua ubunifu, kukuza teknolojia na kusaidia kutafuta majawabu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, hivyo ni muhimu kwa wadau kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za utafiti.
Waziri huyo pia ametangaza kuwa dirisha la kupokea machapisho ya tafiti litafunguliwa kuanzia Juni 19 hadi Oktoba 31 mwaka 2026, ili kuwapa watafiti fursa ya kuwasilisha kazi zao zitakazoweza kuendelezwa na kutumika katika kuharakisha maendeleo ya nchi.