Wananchi watakiwa kuungana vita dhidi ya ukatili wa kijinsi
27 July 2026, 16:32

Kwa kuendelea kutoa elimu na kushirikisha wananchi kupitia majukwaa mbalimbali ya kijamii, Jeshi la Polisi linaamini kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaweza kupungua na jamii ikaendelea kuwa salama kwa kila mtu.
Na Anwary Shaban.
Jeshi la Polisi kupitia Dawati la Jinsia na Watoto limewataka wananchi kuungana katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia, likisisitiza kuwa jukumu la kuzuia vitendo hivyo ni la kila mwananchi ili kujenga jamii salama na yenye usawa.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kigoma, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Polisi Michael Mjema, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ufunguzi wa Tamasha la 17 la Muziki wa Chigogo lililofanyika katika Viwanja vya Chamwino Arts Centre (CAC), mkoani Dodoma.
Mjema amesema matamasha yanayokusanya idadi kubwa ya wananchi ni jukwaa muhimu kwa Jeshi la Polisi kupitia falsafa ya Polisi Jamii kufikisha elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia na kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo hivyo.
Wakati huo huo, baadhi ya wananchi na wakazi wa Mwatano jijini Dodoma waliozungumza na Taswira ya Habari wameeleza kuwa ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu haki za binadamu, usawa wa kijinsia na madhara ya ukatili ni miongoni mwa sababu zinazochochea kuendelea kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.
Aidha, Mjema amesema maelekezo ya viongozi wa Jeshi la Polisi ni kuhakikisha elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia inawafikia wananchi kuanzia ngazi ya wilaya, tarafa, kata, vijiji hadi vitongoji, hatua ambayo inalenga kuongeza uelewa wa jamii na kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.