Jamii yatakiwa kushirikiana kulinda haki za watoto wenye ulemavu
23 September 2026, 16:54

Baadhi ya wananchi wameunga mkono kauli hiyo, wakisema jamii haipaswi kuwatenga watoto wenye ulemavu, bali inapaswa kuwatambua kama sehemu ya jamii na kuhakikisha wanapatiwa haki zao za msingi.
Na Daniel Njau.
Jamii imetakiwa kuhakikisha watoto wenye ulemavu wanapata haki zao za msingi, ikiwemo elimu, malezi na kushirikishwa katika shughuli za kijamii, badala ya kuwafungia ndani au kuwatumia kama njia ya kujipatia kipato.
Akizungumza kuhusu wajibu wa jamii, Bwana Enock Isaya Mbawa, mjumbe wa Kamati Tendaji ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Dodoma, amesema watoto wenye ulemavu ni sehemu ya jamii na wanapaswa kutendewa sawa na watoto wengine bila ubaguzi wala kutengwa.
Mbawa amesema jamii ina nafasi kubwa ya kuhakikisha watoto hao wanapata mahitaji muhimu, ikiwemo kuchangia pale familia inapokosa uwezo wa kugharamia mahitaji ya mtoto yanayohusiana na elimu, ili kuhakikisha haki yao ya kupata elimu inatekelezwa.