Wakazi Chilwana wadai stahiki zao kupisha upanuzi wa barabara
29 October 2026, 17:00

Miundombinu ya barabara ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya miji, kurahisisha usafiri na kuimarisha shughuli za kiuchumi, lakini utekelezaji wa miradi hiyo unahitaji pia kuzingatia haki za wananchi wanaopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi. Kwa wananchi waliokabidhi maeneo yao wakitarajia kulipwa fidia, kuchelewa kwa malipo kunaweza kuwa changamoto katika kupanga upya maisha na shughuli zao za kiuchumi.
Na Victor Chigwada.
Wakazi 18 wa Kitongoji cha Chilwana, Mtaa wa Ihumwa C jijini Dodoma, wameiomba Serikali kuharakisha malipo ya fidia ya maeneo yao yaliyotumika katika mradi wa upanuzi wa Barabara ya Mzunguko ya Nje ya Jiji la Dodoma, wakisema wamekuwa wakisubiri stahiki zao tangu mwaka 2023.
Wakazi hao wamesema muda mrefu umepita tangu waahidiwe kulipwa fidia hizo bila kupata malipo, hali iliyowafanya kuiomba Serikali kuingilia kati ili kuhakikisha wanapata haki zao.
Akizungumza na Taswira ya Habari, mwakilishi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) jijini Dodoma, Colman Gaston, amekiri kupokea malalamiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali, yakiwemo ya Kitongoji cha Chilwana.
Amesema tathmini ya maeneo yaliyotumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo imekamilika na taarifa kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya hatua za malipo ya fidia kwa wananchi ambao bado hawajalipwa.
Serikali ilitenga jumla ya Shilingi bilioni 17 kwa ajili ya fidia za mradi wa Barabara ya Mzunguko ya Nje ya Jiji la Dodoma, yenye urefu wa kilomita 112.3. Kati ya fedha hizo, takribani Shilingi bilioni 12.76 zilikuwa zimelipwa kwa wananchi 2,338 waliokuwa wameidhinishwa kupata fidia.
Mradi huo unahusisha vipande viwili vya barabara, Nala–Veyula–Mtumba–Ihumwa na Ihumwa–Matumbulu–Nala, na kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, utekelezaji wake ulikuwa umefikia takribani asilimia 92.