Dodoma FM

Mila, desturi zatajwa kuchangia malezi na maadili kwa vijana

20 October 2026, 16:52

Picha ni vijana wakidumisha mila na desturi za jamii yao. Picha na Vijimambo.

Mila na desturi za Kiafrika zimetajwa kuwa na mchango mkubwa katika kujenga malezi bora na kukuza maadili mema kwa vijana, ikiwemo kuwafundisha heshima, uwajibikaji, nidhamu na kuthamini watu wazima katika jamii. Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza kuwa kupungua kwa uzingatiaji wa mila na desturi za makabila yao, sambamba na athari za utandawazi, kumechangia mabadiliko ya tabia na mwenendo wa vijana, hali inayozua haja ya wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kuimarisha malezi yanayozingatia misingi ya utamaduni na maadili mema bila kupuuza mabadiliko chanya ya wakati uliopo.

Na Victory Chigwada.

Kupungua kwa uzingatiaji wa baadhi ya mila na desturi za jamii kumetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia mabadiliko ya maadili kwa vijana, huku wazee wakihimiza familia kuendeleza tamaduni zenye mchango katika malezi, heshima na uwajibikaji kwa jamii.

Baadhi ya wananchi wamesema vijana wa sasa wanakosa fursa za kujifunza mila na desturi za makabila yao, hali wanayoieleza kuwa inachangia kupungua kwa heshima kwa watu wazima na kudhoofisha urithishaji wa tamaduni kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Wameongeza kuwa utandawazi umeongeza mwingiliano wa tamaduni za kigeni, hivyo kuna haja ya kuhifadhi mila na desturi zenye manufaa kwa jamii.

Mzee wa kimila katika Mtaa wa Mapinduzi A, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Golden Mathayo, amesema mabadiliko ya maisha yamechangia baadhi ya watoto kushindwa kujifunza lugha za makabila ya wazazi wao na kutumia zaidi Kiswahili, hali inayoweza kudhoofisha urithishaji wa utamaduni wa jamii husika.

Mathayo ameongeza kuwa kupungua kwa baadhi ya mila za jadi, ikiwemo jando lililokuwa likifanyika porini, kumechangia maeneo yaliyokuwa yakitumika kwa shughuli hizo kupoteza umuhimu wake wa kimila. Amesisitiza umuhimu wa jamii kuhifadhi na kurithisha mila na desturi zenye manufaa kwa malezi na utambulisho wa vizazi vijavyo

Simulizi na Victory Chigwada.