DEKALB yatoa mbinu kwa wakulima Kelema jinsi ya kuongeza mazao
23 November 2026, 17:32

Kwa hakika, elimu ya kilimo bora ni nyenzo muhimu katika kuongeza uzalishaji na kumuinua mkulima kiuchumi.
Na Mariam Kasawa.
Imeelezwa kuwa mafanikio ya kilimo cha mahindi hayategemei ukubwa wa shamba pekee, bali pia uchaguzi sahihi wa mbegu zinazoweza kuhimili mazingira ya eneo husika na kutoa mavuno bora.
Hayo ni miongoni mwa mambo yaliyowaleta pamoja wakulima wa kijiji cha Kelema, wilayani Chemba, mkoani Dodoma, ili kupata elimu ya utambuzi na matumizi sahihi ya mbegu bora za mahindi zinazozalishwa na kampuni ya Dekalb.
Wakulima hao wamepatiwa elimu hiyo kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu aina mbalimbali za mbegu za mahindi, namna ya kuzitambua mbegu halisi pamoja na kuchagua mbegu zinazofaa kwa mazingira yao, hatua inayolenga kuimarisha kilimo biashara na kuongeza tija katika uzalishaji.
Akizungumza na wakulima hao, Bwana Benson Kimaro, ambaye ni Bwana Shamba wa kampuni ya Delkab mkoani Dodoma, ameeleza aina mbalimbali za mbegu zinazozalishwa na kampuni hiyo na kueleza namna wakulima wanavyoweza kuchagua mbegu zinazowafaa ili kupata mavuno bora.
Aidha, Kimaro amefafanua alama na viashiria vinavyopaswa kuangaliwa wakati wa kununua mbegu za Delkab, akiwataka wakulima kuwa makini na kuhakiki uhalisia wa mbegu wanazonunua ili kuepuka kuuziwa mbegu bandia zinazoweza kusababisha hasara katika uzalishaji.
Kwa upande wake, Subira Salum, ambaye ni mkulima wa mfano, balozi na mtumiaji wa mbegu za Delkab, amesema amekuwa akitumia mbegu hizo kwa zaidi ya miaka minne, akieleza namna matumizi yake yalivyomnufaisha katika shughuli za kilimo.
Aidha, amewahimiza wakulima wengine kutumia mbegu bora na kufuata ushauri wa kitaalamu ili kuongeza mafanikio katika kilimo.

Nao baadhi ya wakulima walioshiriki mafunzo hayo wameeleza namna elimu waliyoipata itakavyo wasaidia kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi na matumizi ya mbegu msimu huu wa kilimo, wakibainisha kuwa uelewa huo utawawezesha kuepuka changamoto walizokuwa wakikabiliana nazo awali.
Wakulima wanahimizwa kuzingatia ushauri wa wataalamu, kununua mbegu kutoka kwa wauzaji wanaoaminika na kuhakikisha wanatumia mbegu zinazofaa kwa mazingira yao ili kujenga kilimo chenye tija na kukuza uchumi wa kaya na Taifa.