Wazazi wahimizwa kuwekeza katika elimu ya watoto
20 November 2026, 17:02

Jamii imetakiwa kuweka kipaumbele katika elimu ya watoto kwa kuwajengea msingi imara wa maarifa tangu wakiwa wadogo, ili kuwaandaa kukabiliana na mabadiliko ya dunia ya sasa inayotegemea kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Na Victor Chigwada.
Akizungumza na wazazi katika mahafali ya watoto wa elimu ya awali inayotolewa katika msikiti wa ihumwa jijini dodoma, katibu wa msikiti huo, majdi ally, amesema mzazi anapaswa kutambua kuwa mtoto ni sehemu muhimu ya mustakabali wa familia na taifa, hivyo ana wajibu wa kumwandaa kwa kumpatia elimu itakayokuwa msingi wa maisha yake ya baadaye.
Amesema katika dunia ya sasa, elimu ni nyenzo muhimu katika nyanja mbalimbali za maisha, iwe ni kilimo, biashara, uongozi au shughuli nyingine za kiuchumi, hivyo wazazi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata maarifa yatakayowawezesha kujitegemea na kushiriki katika maendeleo ya jamii.
Aidha, ally amesisitiza kuwa malezi ya kielimu kwa watoto hayapaswi kuishia katika elimu ya darasani pekee, bali yanapaswa kuhusisha pia elimu ya dini ili kuwajengea misingi ya maadili, nidhamu na uwajibikaji itakayowasaidia kuwa raia wema na wenye mchango chanya katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi wameunga mkono umuhimu wa elimu kwa watoto, wakieleza kuwa elimu ni urithi muhimu ambao mzazi anaweza kumwachia mtoto wake.
Wamesisitiza kuwa jukumu la kumjengea mtoto msingi wa elimu na maadili linapaswa kuanzia nyumbani kabla hata hajaanza masomo rasmi, ili kumwandaa kuwa mtu mwenye maarifa na misingi bora ya maisha.