Dodoma FM

Shughuli za nyumbani zatajwa kujenga uwajibikaji kwa watoto

3 November 2026, 16:27

Picha ni wazazi wakiwafundisha watoto majukumu mbalimbali katika familia. Picha na Dodoma fm.

Malezi ya watoto yanahitaji uwiano kati ya kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kulinda haki zao za kukua katika mazingira salama. Kuwashirikisha watoto katika majukumu madogo ya nyumbani na shughuli zinazolingana na umri wao kunaweza kuwajengea nidhamu, uwajibikaji na ujuzi wa maisha, lakini wanapopewa kazi nzito au zinazochukua muda mwingi zinaweza kuathiri afya, maendeleo yao na ushiriki wao katika masomo.

Na Daniel Njau.

Wazazi na walezi wametakiwa kuwashirikisha watoto katika shughuli ndogondogo za nyumbani kama sehemu ya malezi yanayowajengea uwajibikaji, bidii na uwezo wa kujitegemea, huku wakizingatia umri na uwezo wao ili majukumu hayo yasiathiri haki zao za msingi, ikiwemo kupata elimu, kucheza na kupumzika.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu suala hilo, wakitafsiri kuwapa watoto majukumu ya nyumbani kama aina ya ajira isiyo na malipo, huku wengine wakiona ni njia sahihi ya kuwafundisha stadi za maisha, zikiwemo kufua, kufagia na kufanya usafi.

Mlezi katika kituo cha watoto, Bwana Dastan Haule amesema kufanya shughuli hizo ni sehemu ya makuzi ya mtoto kwa kuwa humsaidia kujenga uwezo wa kufanya kazi na kushiriki katika majukumu ya kijamii. Amesisitiza kuwa majukumu hayo hayapaswi kuathiri haki ya mtoto kupata muda wa kusoma, kucheza na kushiriki shughuli nyingine muhimu kwa ukuaji wake.

Ameeleza kuwa pale majukumu yanapomnyima mtoto muda wa kutekeleza mahitaji yake ya msingi, yanavuka mipaka ya malezi na kuanza kufanana na ajira ya mtoto. Hivyo, ameshauri wazazi kupewa elimu kuhusu shughuli zinazofaa kufanywa na watoto kulingana na umri na uwezo wao, bila kuhatarisha ustawi wao.

Kwa upande wake, Mwalimu Godfrey Amosi, mwalimu wa shule ya awali, amesema shuleni kumekuwa na utaratibu wa kuwafundisha watoto kujitegemea kupitia shughuli mbalimbali zinazolingana na umri wao.

Ripoti ya Daniel Njau.