Wakazi ihumwa wadai ukarabati wa barabara kabla ya mvua
22 October 2026, 16:27

Msimu wa mvua unapokaribia, hali ya barabara huwa changamoto kwa wananchi wanaotegemea miundombinu hiyo kufika kazini, kusafirisha bidhaa na kupata huduma muhimu za kijamii. Barabara zisizokuwa katika hali nzuri zinaweza kuharibika zaidi kutokana na maji ya mvua, na kusababisha usafiri kuwa mgumu au kukatika kabisa katika baadhi ya maeneo.
Na Victory Chigwada.
Wakazi wa Mtaa wa Ihumwa jijini Dodoma wameiomba Serikali kukarabati barabara inayopita katika eneo hilo kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua, wakieleza kuwa hali ya barabara hiyo huzorota wakati wa mvua na kusababisha usafiri kuwa mgumu.
Wakizungumza na chombo hiki, wananchi hao wamesema barabara hiyo huharibika na kuwa na mashimo wakati wa mvua, hali inayowapa usumbufu watumiaji wa barabara na kuathiri shughuli zao za kila siku. Wameiomba mamlaka husika kuchukua hatua mapema ili kupunguza changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Dodoma Jiji, Mhandisi Emanuel Mfinanga, amekiri kuwepo kwa maelekezo ya barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami, akieleza kuwa jukumu hilo lilipokelewa na TANROADS.
Amesema kwa sasa wanasubiri kibali na fedha kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi huo, huku akiahidi kuwa TARURA itaendelea kufanya ukarabati wa barabara hiyo kabla ya mvua kuanza ili kurahisisha usafiri wakati wananchi wakisubiri ujenzi wa kiwango cha lami.