Mazoezi kinga dhidi ya magonjwa na msongo wa mawazo
4 November 2026, 17:01

Wataalamu wa afya na mazoezi wamewahimiza wananchi kuzingatia kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku, wakieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuimarisha afya ya akili na kuboresha ustawi wa mwili kwa ujumla.
Na Daniel Njau.
Wakizungumzia umuhimu wa mazoezi hayo, wataalamu wamesema kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30 kwa siku kuna mchango mkubwa katika kuimarisha misuli na mfumo wa moyo, kudhibiti uzito wa mwili pamoja na kupunguza hatari ya kupata magonjwa mbalimbali, yakiwemo shinikizo la damu, kisukari na magonjwa ya moyo.
Kwa upande wake, Dkt. Francis Mabele, Daktari wa Viungo, amesema mazoezi ya mwili yana nafasi muhimu katika kulinda afya ya akili, kwani husaidia kupunguza msongo wa mawazo na wasiwasi, huku yakichangia kuboresha ubora wa usingizi.
Ameongeza kuwa watu wanaojenga utaratibu wa kufanya mazoezi mara kwa mara wanaweza kuimarisha uwezo wa kuzingatia shughuli zao za kila siku na kudumisha uwiano mzuri wa afya ya mwili na akili.
Wakieleza uzoefu wao, baadhi ya wananchi wamesema wameanza kujumuisha mazoezi katika ratiba zao za kila siku na kubaini mabadiliko chanya, yakiwemo kuongezeka kwa nguvu na uwezo wa kutekeleza shughuli za kazi, kupungua kwa uchovu pamoja na kuboreka kwa afya zao kwa ujumla.