Vijana watakiwa kutumia fursa kujikwamua kiuchumi
1 October 2026, 17:11

Vijana wanahimizwa kuwa wabunifu na wenye juhudi katika kutafuta njia za kujipatia kipato, kwa kutumia ujuzi walionao pamoja na fursa zinazopatikana kupitia teknolojia. Hatua hiyo inaonekana kuwa muhimu katika kupunguza utegemezi na kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, huku mafanikio yakihitaji uvumilivu, mipango na kuanza kuchukua hatua badala ya kusubiri nafasi za kuajiriwa.
Na Victor Chigwada.
Vijana wametakiwa kutumia maarifa, ujuzi na nguvu walizonazo katika kukabiliana na changamoto za maisha, ikiwemo ukosefu wa ajira, badala ya kusubiri kuajiriwa.
Imeelezwa kuwa pamoja na kuwepo kwa fursa mbalimbali zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya mitandao ya kijamii, baadhi ya vijana bado hawajatumia fursa hizo ipasavyo katika kujiajiri na kuongeza kipato.
Akizungumza na vijana, mhitimu wa masomo ya Theolojia, Happy Makangala, amesema vijana wanapaswa kutambua kuwa juhudi wanazoweka leo ndizo msingi wa mafanikio yao ya kesho, hivyo ni muhimu kutumia fursa zilizopo badala ya kukaa na kusubiri ajira.