Dodoma FM

Shule ya sekondari Mpwapwa kutimiza miaka 100

17 August 2026, 17:45

Shule hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwaandaa watoto wa machifu ili baadaye waweze kurithi.Picha na Stephen Noel.

Shule ya Sekondari Mpwapwa inatarajiwa kuadhimisha miaka 100 ya uwepo wake mwaka 2026, ikiwa ni kumbukumbu ya safari yake ya karne moja katika sekta ya elimu nchini.

Na Stephen Noel

Shule ya Sekondari Mpwapwa, iliyopo katika Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, inatarajia kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1926, wakati wa utawala wa kikoloni.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mpwapwa, Mwalimu Omary Twakal, amesema shule hiyo ilianzishwa kwa lengo la kuwaandaa watoto wa machifu ili baadaye waweze kurithi na kutekeleza majukumu mbalimbali ya kiutawala baada ya kumalizika kwa utawala wa kikoloni.

Amesema katika kipindi cha miaka 100, shule hiyo imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kutoa elimu na kuandaa wataalamu mbalimbali ambao wameitumikia jamii na taifa kwa ujumla.

Hata hivyo, pamoja na shule hiyo kufikisha historia ya miaka 100, bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali za miundombinu.

Felex Malimbo, Mkuu wa Kitengo cha Ukarabati shuleni hapo, amesema miongoni mwa changamoto zinazohitaji kushughulikiwa ni pamoja na ukosefu wa uzio wa shule, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa wanafunzi na mali zao, hususan katika mabweni.

Amesema pia shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya usafiri, hivyo kuhitajika kwa jitihada zaidi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Kwa upande wao, wanafunzi wa shule hiyo wameiomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya TEHAMA, ikiwemo kuanzishwa au kuboreshwa kwa darasa la kompyuta, ili waweze kupata elimu inayokwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Wamesema maboresho hayo yatasaidia kuongeza ujuzi wa wanafunzi katika matumizi ya teknolojia na kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.

Sauti ya habari kamili