Mgogoro wa ardhi wapelekea nyumba kubomolewa
3 September 2026, 15:52

Huku kila upande ukisisitiza kuwa una haki ya kumiliki eneo hilo, kinachosubiriwa sasa ni ufafanuzi wa mwisho wa mamlaka za Serikali kuhusu umiliki halali wa ardhi hiyo na hatua zitakazofuata.
Na Anwary Shaban
Mgogoro wa umiliki wa ardhi katika eneo la Kikuyu Extension jijini Dodoma umeingia sura mpya baada ya nyumba ya mkazi mmoja, Raheli Sule, kubomolewa kufuatia mvutano wa umiliki wa eneo hilo.
Raheli anadai kuwa alijenga nyumba hiyo mwaka 2012, kabla ya eneo hilo kupimwa rasmi mwaka 2016, na kwamba anazo nyaraka anazodai kuthibitisha umiliki wake wa ardhi hiyo.
Akizungumza akiwa katika eneo la Kikuyu Extension jijini Dodoma, Raheli Sule ameeleza kuwa hadi mwaka 2023 alikuwa amekamilisha malipo yote yaliyohitajika katika umiliki wa eneo hilo, huku akisubiri taarifa zake za umiliki kuingizwa katika mfumo mpya wa usajili wa ardhi.

Hata hivyo, upande mwingine wa mgogoro huo unadai kuwa eneo hilo linamilikiwa kihalali na Bi. Adelaide Koko, ambaye anasema hatua ya kubomoa nyumba hiyo haikufanyika kwa maamuzi ya mtu binafsi, bali ni utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Serikali.
Akizungumzia mgogoro huo waziri wa Ardhi, Dkt. Leonard Akwilapo, amesema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi imechukua msimamo wake kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazohusu umiliki na matumizi ya ardhi nchini.
Mgogoro huo unaibua maswali kuhusu historia ya umiliki wa eneo hilo, uhalali wa nyaraka zinazomilikiwa na kila upande, pamoja na hatua zilizochukuliwa na mamlaka kabla ya nyumba hiyo kubomolewa.