Wazazi Mapinduzi watakiwa kushiriki maendeleo ya shule
8 June 2026, 18:07

Serikali imekuwa ikisisitiza kuwa hakuna mwanafunzi anayepaswa kufukuzwa, kuzuiwa kufanya mtihani au kunyimwa huduma za msingi kwa sababu ya kutotoa mchango wa hiyari.
Na Elizabeth Tanzania.
Wazazi na walezi katika Kijiji cha Mapinduzi A Jijini Dodoma wametakiwa kuendelea kushiriki katika utoaji wa michango ya hiari kwa ajili ya maendeleo ya Shule ya Msingi Nguji, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Akizungumza na Taswira ya Habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Nguji, Zakayo Mgogoro, amesema michango hiyo imekuwa na tija kubwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za shule, ikiwemo kugharamia chakula cha wanafunzi, kulipa walimu wa kujitolea pamoja na kuendesha mitihani ya majaribio kwa madarasa ya mitihani.
Ameeleza kuwa licha ya baadhi ya wazazi kuitikia vyema wito huo, bado kuna wazazi wachache ambao hawajashiriki kikamilifu katika michango hiyo, hali inayoweza kuathiri utekelezaji wa baadhi ya shughuli za maendeleo ya shule.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo wamesema michango ya hiari imekuwa na manufaa makubwa kwa watoto wao, kwani imechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ari ya wanafunzi katika masomo.
Wakitoa wito kwa wazazi na walezi wengine, wananchi hao wamewataka kuona umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya watoto wao kupitia michango ya hiari inayokubalika kisheria kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa mujibu wa mwongozo wa Elimu Bila Ada na Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016, michango ya maendeleo ya shule inaruhusiwa pale inapokubaliwa na vikao halali vya shule na jamii husika, ikiwa ni ya hiari na isiyomnyima mwanafunzi haki ya kupata elimu kwa kushindwa kuchangia.