Dodoma FM

Wananchi waonywa kuacha tabia ya kuvaa miwani bila kufanyiwa uchunguzi

29 June 2026, 18:04

Hali hiyo imekuja kufuatia kuongezeka kwa matumizi ya miwani ya macho katika jamii.Picha na Mtandao.

Katika kupambana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Bodi ya Optometria, inatekeleza Sheria ya Optometria Sura ya 23 ya mwaka 2007, inayosimamia huduma za macho nchini kwa kuhakikisha vipimo na uuzaji wa miwani ya macho unafanywa na wataalamu waliothibitishwa ili kulinda afya ya wananchi.

Na Husna Munis.

Wataalamu wa afya ya macho wameonya dhidi ya tabia ya baadhi ya watu kuvaa miwani ya macho bila kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu, wakieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuathiri uwezo wa macho kuona kwa usahihi.

Hali hiyo imekuja kufuatia kuongezeka kwa matumizi ya miwani ya macho katika jamii, ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitumia miwani kwa urembo bila kujua madhara yake kiafya.

Akizungumza, Daktari wa Macho kutoka Kliniki ya Macho CVT iliyopo Nyasubi, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Saidi Msabaha, amewataka wananchi kuhakikisha wanapima macho na kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kutumia miwani ya macho.

Amesema matumizi ya miwani bila vipimo sahihi yanaweza kusababisha matatizo mbalimbali yakiwemo maumivu ya kichwa, kizunguzungu, na hata kuathiri ukuaji wa uwezo wa kuona, hususan kwa watoto ambao macho yao bado yanakua.

Sauti ya Dkt Nyasubi.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wamesema kumekuwa na tabia ya watu kutumia miwani ya macho bila ushauri wa wataalamu, hali wanayodai inaweza kuhatarisha afya ya macho, wakisisitiza kuendelea kwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya miwani hiyo.

Sauti za wananchi.