Dodoma FM

Wafanyabiashara watakiwa kutoa ushirikiano kwa jeshi Zimamoto

18 June 2026, 17:43

Wananchi wametakiwa kuendelea kutumia namba ya dharura 114 kutoa taarifa za matukio ya moto na dharura.Picha na Dodoma fm.

Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina jukumu la kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari za moto katika maeneo mbalimbali ili kuzuia majanga na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.

Na Elizabeth Tanzania.

Wafanyabiashara mkoani Dodoma wamehimizwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakati wa ukaguzi wa kinga na tahadhari dhidi ya majanga ya moto ili kuimarisha usalama wa maisha na mali zao.

Akizungumza na Taswira ya Habari, Afisa Habari, Uhusiano, Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mrakibu Msaidizi (ASF) Steven Kate amesema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakikwepa ukaguzi huo au kutoa taarifa zisizo sahihi kwa hofu ya gharama zinazohusiana na tozo za huduma hizo.

Amesema hali hiyo inaweza kuongeza hatari ya kutokea kwa majanga ya moto na kusababisha hasara kubwa ambazo zingeweza kuzuilika kama hatua za kinga na tahadhari zingechukuliwa mapema.

Sauti ya (ASF) Steven Kate.

Aidha, ASF Kate amesisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kushirikiana na maafisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wanapofanya ukaguzi, ili kubaini mapungufu ya kiusalama na kuyafanyia kazi kabla hayajasababisha madhara.

Pia amewakumbusha wananchi kuendelea kutumia namba ya dharura 114 kutoa taarifa za matukio ya moto na dharura nyingine zinazohitaji huduma za uokoaji kwa wakati.

Sauti ya (ASF) Steven Kate.