Mradi wa maendeleo jumuishi ya kijani wazinduliwa Dodoma
19 June 2026, 18:26

Agridiversity Tanzania ni shirika lisilo la kiserikali (NGO) la Tanzania linalojihusisha na kuendeleza kilimo endelevu kwa wakulima wadogo.
Na Elizabeth Tanzania.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amezindua Mradi wa Maendeleo Jumuishi ya Kijani (Inclusive Green Transformation – IGRET), unaolenga kuimarisha uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi na wakulima kupitia matumizi endelevu ya rasilimali za asili.
Mradi huo unaowezeshwa na Save the Children Tanzania kwa ufadhili wa European Union, unalenga kuhamasisha mbinu za kilimo zinazosaidia utunzaji wa mazingira, na kuwajengea wakulima uwezo wa kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo jijini Dodoma, Senyamule amesema mradi huo umekuja katika kipindi ambacho mkoa huo unaendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa ajira,athari ya mabadiliko ya tabianchi,matumizi hafifu ya teknolojia katika kilimo na upatikanaji mdogo wa mitaji kwa vijana hivyo mradi huo huo utakuwa chachu kwa maendeleo.

Aidha, amesisitiza ushiriki wa vijana mbalimbali katika mradi huo na majukwaa ya sera na maamuzi yanayohusu maendeleo yao wenyewe .
Kwa upande wake mwanzilishi na mwenyekiti wa taasisi ya Agridivesity Tanzania Stephano Msuya amewataka vijana kutumia fursa ya uwepo wa taasisi hiyo kuonyesha utaalam walio nao kwa manufaa ya jamii.