Wananchi wa Chang’ombe watakiwa kutunza miradi ya maendeleo
16 July 2026, 16:47

Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kutathmini ubora wa kazi zinazofanyika na kuhakikisha miradi hiyo inakidhi viwango vinavyotarajiwa pamoja na kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Na Anwary Shaban.
Wananchi wa Kata ya Chang’ombe watakiwa kuendelea kuitunza na kuilinda miradi mbalimbali ya maendeleo ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Hayo yamesemwa na Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bakari Fundikira mara baada ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Chang’ombe Jijini Dodoma.
Amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza fedha nyingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye lengo la kuboresha huduma za kijamii na kuinua ustawi wa wananchi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika kuilinda na kuitunza.
Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na Serikali ni msingi muhimu wa kuhakikisha uwekezaji unaofanywa unaendelea kuleta matokeo chanya katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, miundombinu na huduma nyingine za kijamii.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Chang’ombe, Hussein Kabezi alisema kuwa wanaishukuru serikali kwa ujenzi wa miradi katika kata ya Chang’ombe kwani imekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi.