𝗦heria ya elimu ni nyenzo ya utekelezaji wa mageuzi ya elimu nchini
21 May 2026, 17:30

Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wa elimu kutoka sekta tofauti, huku serikali ikionesha dhamira ya kuendelea kufanya maboresho ya sera na sheria za elimu kwa maslahi ya wanafunzi, walimu na taifa kwa ujumla.
Na Mwandishi wetu.
Mageuzi ya elimu nchini yanahitaji mfumo imara wa kisheria utakaowezesha utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la 2023 na mitaala iliyoboreshwa.
Hayo yameelezwa Mei 21, 2026 jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika Kikao cha kujadili taarifa ya awali ya mapitio ya Sheria ya Elimu Sura 353 ambapo amesema maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mageuzi ya elimu yameweka msingi wa maboresho ya sera, mitaala na sheria.
Aidha amesisitiza kuwa ushirikishwaji wa wadau ni muhimu ili kupata maoni yatakayo saidia kuimarisha mfumo wa elimu.

Naye Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi naTeknolojia, mh.Wanu Hafidhi Ameir amesema madhumuni makuu ya kikao hicho ni kusikiliza taarifa ya awali ya mapitio ya sheria ya elimu ambayo bado haijawa rasimu rasmi.
Amesema ana imani wadau wataendelea kushiriki kikamilifu kwa kutoa maoni yatakayo saidia kuboresha sekta ya elimu nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi naTeknolojia, Caroline Nombo amewahakikishia wadau kuwa maoni yote yatakayo kusanywa yatafanyiwa kazi kwa kina ili kupata maboresho yenye tija katika sekta ya elimu.
Aidha, amewataka wadau kuwa wazi na kushiriki kikamilifu ili kupata mawazo bora zaidi yatakayo saidia maendeleo ya elimu pamoja na kuimarisha mawasiliano kati ya serikali na wadau wa elimu.