Dodoma FM

Vijiji vyote kupatiwa umeme katika awamu ya tatu ya REA

9 April 2021, 9:59 am

Na; Yussuph Hans.

Serikali imesema inawahakikishia Wananchi wa maeneo yote ya Vijijini  yaliyokuwa hayajapata Umeme katika awamu zilizopita kuwa, yatapata Umeme katika awamu ya Tatu ya mzunguko huu wa pili wa REA .

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati Stephen Byabato alipokuwa akijibu swali la Nyongeza  la Mh. Kunti Yussuph Majala Mbunge wa Viti Maalumu  lililohoji Serikali ina mpango gani wa kufikisha umeme katika Vijiji vya kata ya Handa,Sanzawa na Mpendo Wilayani Chemba katika awamu ya tatu ya REA.

Akijibu swali hilo Mh. Byabato amesema kuwa vijiji vyote ambavyo havijapata Umeme katika awamu ya pili ya mzunguko wa pili wa REA, Serikali imeviweka katika mpango maalumu navyo ni takribani  1900 ambavyo vitapatiwa umeme bila kuacha kijiji hata kimoja.

Akijibu swali la pili la nyongeza la Mh Kuntu Majala kuhusu Serikali kuwalipa Wananchi mali zao zinapoharibika kutokana na ukatikaji wa umeme bila taarifa maeneo mbalimbali ikiwemo wilayani chemba, Mh Byabato amesema kuwa, changamoto kubwa  inayo ukabili Mkoa wa Dodoma ni  kuwa na udongo tepetepe unao pelekea nguzo nyingi kudondoka msimu wa mvua  hivyo wametatua tatizo hilo kwa kuanza kuweka nguzo za zege zinazo himili hali hiyo.

Sanjari na hayo Mh Byabato amesema kuwa Serikali ina Mpango wa kujenga vituo vidogo vya Umeme Vinne (substation) ambavyo vitahudumia Mkoa wa Dodoma na kupunguza mahitaji ya Umeme na kuwepo kwa Umeme wa uhakika.