Dodoma FM

Kongwa watakiwa kushiriki katika utunzaji wa mazingira

18 January 2024, 8:44 am

Picha ni wadau wa wa mazingira wilayani Kongwa wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti . Picha na Alfred Bulahya.

Zoezi la upandaji miti limehusisha kamati ya usalama ya Wilaya, Wakuu wa Divisheni na Vitengo, wananchi na watumishi ambapo Mhe. Mayeka alipanda mti kama ishara ya uzinduzi wa zoezi.

Na Alfred Bulahya.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amewataka wananchi kushiriki kwenye shughuli za utunzaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na usafi wa kila jumamosi na upandaji miti katika maeneo yao.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti Mhe. Mayeka amezielekeza Taasisi mbalimbali Wilayani Kongwa kuwa na mipango ya muda mrefu ya matumizi ya ardhi, itakayowezesha Taasisi hizo kutunza miti inayopandwa katika maeneo hayo.

Amesema Wilayani kongwa kwa sasa usafi unafanyika Kila Jumamosi badala ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi kama ilivyopangwa kitaifa.

Sauti ya Mhe. Mayeka Simon Mayeka.

Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa taratibu, Wananchi waliopakana na barabara wanawajibika kusafisha hadi barabarani na pia katika siku za usafi wa Mazingira wafanya biashara hawana sababu ya kufunga maeneo yao ya biashara kwani kinachotakiwa ni kuhakikisha mazingira yanayowazunguka yanakuwa katika hali ya usafi.

Picha ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka akiongea katika hafla hiyo ya hafla ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti.Picha na Alfred Bulahya.

Naye Dkt. Omary Nkullo Mkurugenzi Mtendaji amesema Halmashauri imekusudia kupanda miti kwenye eneo lote la Hospitali ya Wilaya lenye ukubwa wa ekari 21, kwa kuwa ipo miche ya kutosha ambapo zaidi ya miti 200 imepandwa katika hafla hiyo.

Sauti ya Dkt. Omary Nkullo.

Akizungumza kikao hicho, Afisa Maliasili na mazingira Bwana Godfrey Mujairi ametaja shughuli za kibinadamu kama changamoto kubwa inayopelekea uharibifu wa Mazingira ikiwemo uvamizi wa misitu na maeneo ya uchimbaji madini, ukataji miti ovyo, kilimo na ufugaji holela na utupaji hovyo taka kando ya barabara.

Sauti ya Bwana Godfrey Mujairi .