Dodoma FM

Wananchi Engusero waandamana kupinga kuondolewa kwenye maeneo yao

14 May 2026, 16:15

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Taswira ya Habari wamedai kuwa hatua ya kupewa taarifa za kuondoka imewashtua.Picha na Kitana Hamis.

Wananchi wa Engusero wameendelea kusubiri majibu na ufafanuzi wa kina kutoka kwa mamlaka husika kuhusu mustakabali wa maeneo yao, huku wakisisitiza kuwa wanahitaji suluhisho la kudumu litakalowawezesha kuendelea kuishi kwa amani na kuendeleza shughuli zao za maendeleo.

Na Kitana Hamis.

Taswira ya Habari imefika katika vitongoji vya Meremere na Nesetani vilivyopo Kijiji cha Engusero, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, ambapo wananchi wa maeneo hayo wameeleza hofu na wasiwasi Yao kufuatia taarifa walizodai kupatiwa za kutakiwa kuondoka katika maeneo wanayoishi ili kupisha shughuli za malisho ya mifugo.

Wananchi hao wamesema wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo kwa muda mrefu huku wakifanya maendeleo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo kujenga makazi ya kudumu, kuanzisha shughuli za kilimo pamoja na kuchangia ujenzi wa huduma muhimu za jamii kama shule, nyumba za ibada na miundombinu mingine inayotumiwa na wakazi wa eneo hilo.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Taswira ya Habari wamedai kuwa hatua ya kupewa taarifa za kuondoka imewashtua, kwani wengi wao hawajui hatima yao endapo wataondolewa katika maeneo hayo bila kupatiwa ufafanuzi wa kina au maeneo mbadala ya kuishi na kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Wananchi hao wameiomba Serikali kuangalia kwa karibu suala hilo na kuhakikisha kuwa maamuzi yoyote yatakayofanyika yanazingatia haki, ustawi na maisha ya wananchi waliopo katika maeneo hayo kwa muda mrefu. Aidha, wameeleza kuwa maendeleo yaliyopo katika vitongoji hivyo ni ushahidi kuwa maeneo hayo yamekuwa yakikaliwa rasmi kwa miaka mingi.

Picha ni wakazi wa Engusero wakiwa wameandamana kupinga tamko hilo.Picha na Kitana Hamis.

Katika hatua nyingine, viongozi wa mila wa eneo hilo walitoa kauli zao mbele ya wananchi, wakisisitiza umuhimu wa amani, mazungumzo na upatikanaji wa suluhisho litakalolinda maslahi ya jamii nzima bila kuleta migogoro kati ya wananchi na mamlaka husika.

Viongozi hao wa mila walieleza kuwa wananchi wa Meremere na Nesetani wamekuwa wakiheshimu sheria na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo ni muhimu kwa mamlaka zinazohusika kusikiliza maoni ya wananchi kabla ya kufikia maamuzi makubwa yanayogusa maisha yao moja kwa moja.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Nesetani alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa eneo hilo, alitoa maelezo kuhusu suala hilo huku akiweka masharti ya kutopigwa picha wakati wa mazungumzo hayo.

Kwa upande wake, Afisa Ardhi wa Wilaya ya Kiteto akizungumza na Taswira ya Habari kwa njia ya simu, alisema ofisi yake inaendelea kufuatilia suala hilo kwa karibu na kwamba hatua zote zinazochukuliwa zitafuata taratibu, sheria na miongozo ya Serikali ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kila upande.