Dodoma FM

Dkt.Mpango apitishwa kuwa makamu wa rais bila kupingwa

30 March 2021, 12:15 pm

Na,Mindi Joseph.

Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Samia Suluhu Hassan amemteua Dk.Phillipo Mpango aliyekuwa waziri wa Fedha na Mipango  kuwa makamu wa Rais na kupitishwa na Bunge kwa asilimia 100.

Jina la Mpango limesomwa Bungeni jijini Dodoma leo na Spika Job Ndugai baada ya kuletewa jina hilo na  mpambe wa Rais Mh.Samia  Suluhu, ambapo jumla ya  wabunge waliopiga kura ni 363 na kumpitisha kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.

Baada ya Dk.Mpango kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais  Baadhi ya wabunge wamempongeza na kumuomba kwenda kusimamia maslahi ya wananchi wanyonge.

Akizungumza mara baada ya uteuzi huo Dkt.Philiph Mpango amemshukuru Rais Mh.Samia Suluhu Hassan kwa kulipendekeza jina lake kuwa Makamu wake na ameahidi kumsaidia kuhakikisha wanakamilisha miradi ya maendeleo na kuwasaidia wananchi wanyonge kwani Zaidi ya watu milion 14 bado wanaishi maisha Duni.

Dkt.Mpango aliteuliwa kuwa mbunge na hayati Dkt.John Pombe Magufuli mwaka 2015-2020 na baadaye kuteuliwa kuwa waziri wa Fedha na Mipango na Mwaka 2020 alitangaza nia ya kuwania Ubunge katika jimbo la Buhigwe Mkoani Kigoma ambapo alipita kwa asilimia 77.

Hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Rais Mteule Mh.Dkt.Mpango itafanyika kesho Ikulu Chamwino Mkoaani Dodoma saa tatu asubuhi.