Dodoma FM

Mhe. Gondwe aagiza Bahi kuongeza Mapato

16 February 2023, 2:44 pm

Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gongwe ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Bahi kuhakikisha inabuni, kusimamia na kuongeza vyanzo vya mapato.Picha na mwananchi

Mkuu wa wilaya ya Bahi Mheshimiwa Godwin Gongwe ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Bahi kuhakikisha inabuni, kusimamia na kuongeza vyanzo vya mapato ili kutekeleza kikamilifu agizo la Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kila wilaya kuhakikisha inakusanya mapato ya kutosha yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa watanzania.

Na Bernad Magawa.

Mheshimiwa Gondwe ameyasema hayo katika kikao cha kwanza alichokutana na wakuu wa Idara zote zilizopo halmashauri ya Wilaya ya Bahi kikilenga kufahamiana, kupokea taarifa ya kila idara pamoja na kupokea maelekezo kutoka kwa Mhe. Gondwe ambaye aliteuliwa hivi karibuni na Mheshimiwa Raisi kuwa Mkuu wa wilaya hiyo, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mkuu wa wilaya ya Bahi.

Mheshimiwa Gondwe.

“Sitarajii kumuona mtu yeyote ambaye atakuwa anapingana na mheshimiwa Raisi na amiri Jeshi mkuu kuhusiana na kuimarisha ukusanyaji wa mapato, agizo hili limetolewa jana na Makamu wa Dkt Philip Mpango, hivyo ni ajenda ya kitaifa na haina mjadala lazima itekelezwe.”

Alisema Gondwe.

Ili kuhakikisha hilo linafanikiwa, ameziagiza idara zote wilayani hapo kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu mikakati waliyojiwekea ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wa wilaya ya Bahi na watanzania kwa ujumla huku akimuagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bahi kubuni vyanzo vipya vya mapato ili halmashauri iwe na mapato ya kutosha.

Mheshimiwa Gondwe.

“ Wilaya ya Bahi ina rasilimali nyingi sana ambazo ni fursa za kuongeza pato la wilaya, tunayo ardhi ambayo lazima tuiongezee thamani ili itunufaishe, tunayo mawe mengi ambayo tukizalisha mradi wa kokoto itakuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa wilaya yetu, tuboreshe maeneo ya minada yetu ili ituzalishie mapato zaidi kwa kuvuta wawekezaji.”

Amesema Gondwe.

Amesema Bahi ina ardhi ya kutosha ambayo ikiongezwa thamani inaweza kuwa chanzo kikubwa cha pato la wilaya huku akimuagiza afisa ardhi wa wilaya hiyo kuhakikisha anatenga maeneo ya uwekezaji ambayo yatavutia wawekezaji mbalimbali kuwekeza Bahi kwani ni wilaya iliyo karibu na Jiji la Dodoma.

Mheshimiwa Gondwe.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bahi Athmani Masasi akipokea maelekezo hayo amesema atahakikisha maagizo yote anayasimamia kikamilifu kuhakikisha wilaya ya Bahi inastawi na kuwa kivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.