Dodoma FM

Tanzania kuendelea kusimamia usawa wa kijinsia

3 March 2022, 3:05 pm

Na; Mariam Matundu.

Tanzania imezihakikishia nchi za Umoja wa Afrika kuendelea kusimamia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika sekta mbalimbali na kuwawezesha kupata fursa katika sekta hizo

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwanaidi Ali Khamis mara baada ya kuwasili nchini akitikokea Ethiopia alikoshiriki Mkutano wa Sita wa Kamati Maalum ya Mawaziri ya Umoja wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake uliofanyika jijini Addis Ababa Ethiopia.

Mhe. Mwanaidi amesema kuwa nchi za Afrika zimetoa msimamo na kauli moja ya kuhakikisha zinasimamia na kuzingatia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana kupitia Sera na Programu ya kukabiliana na maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na mazingira.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa afua mbalimbali za kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana katika Mkutano huo Mhe. Mwanaidi amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua katika kutomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana na uwezeshaji  kwenye nafasi za uongozi na kiuchumi

Aidha Mhe. Mwanaidi ameeleza kuwa lengo la mkutano huo wa Ethiopia ni kuhakikisha kuwa matokeo ya Mkutano 66 wa Kamisheni ya Wanawake Duniani yananufaisha wanawake na wasichana wa mijini na vijijini barani Afrika

Kwa upande mwingine mkutano huo umekubaliana kuanzishwa kwa mfuko wa Maendeleo ya wanawake barani Afrika (Trust Fund for Africa Women) utakaosadia kuwawezesha wanawake na wasichana katika nchi za Afrika kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo itakayowawezesha kufanya bisahara na miradi mbalimbali katika maeneo yao.

Mkutano wa 6 wa Kamati Maalum ya Mawaziri ya Umoja wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake ni mwanzo wa Mkutano 66 wa Kamisheni ya Wanawake Duniani utakaofanyika jijini New York nchini Marekani kuanzia Machi 14, 2022.