Dodoma FM

Vijana wanufaika na Elimu ya usafi

15 April 2021, 12:23 pm

Na; Mindi Joseph

Jumla ya vijana elfu arobaini na nane Nchini wametajwa kunufaika na  elimu ya usafi inayotolewa na  Taasisi ya Raleigh Tanzania kupitia mradi wa vijana na mabadiliko chanya kitabia juu ya usafi.

Akizungumza na Taswira ya habari mratibu wa mradi huo Augustino Dickson amesema mradi unalenga kuleta mabadiliko chanya ya kitabia kwa vijana na unatekelezwa katika  Mikoa 4  nchini ambayo ni  Dar es  Salaam, Dodoma, Morogoro na Iringa na unahusisha zaidi vijana.

Kampeni hiyo imeanza mwezi Novemba mwaka jana na inatekelezwa kwa miezi 6 na vijana wengi wanaendelea kunufaika na elimu hiyo kwa kuwa pia inawainua kiuchumi.

Kwa upande wao baadhi ya vijana ambao ni wahamasishaji wa masuala ya usafi wamesema  kuwa kampeni hii  inalenga Zaidi  kuwapatia vijana elimu ya usafi  ili  waweze kufahamu njia mbalimbali za kuepuka  na kujikinga  na magonjwa ya mlipuko.

Wakati huo Taasisi ya Raleigh Tanzania leo imefanya usafi katika soko la Chang’ombe na kukakabidhi mafangio 10, vifaa vikubwa vitano vya kuhifadhia taka, reki za kuvutia uchafu 3,  sabuni za kunawia mikono 3 na vitabu  18 vinavyoelezea usafi na kuhitimisha katika shule ya  Sekondari Dodoma kwa kufanya tamasha la usafi na wanafunzi.