Dodoma FM

Jiji laboresha miundombinu ya maji

17 March 2021, 1:47 pm

Na, Alfred Bulahya,

Dodoma.

Halmashauri ya jiji la Dodoma imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 1 kwaajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya maji na barabara ndani ya jiji.

Fedha hizo zimetengwa kupitia bajeti ya mwaka 2021/2022 wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilicholenga kupitisha bajeti hiyo ambayo itatekelezwa kupitia RUWASA na wakala wa barabara mijini na vijijini TARURA.

Akizungumza na Taswira ya habari mkurugenzi wa jiji la Dodoma Bw. Joseph Mafuru amesema hatua hiyo imeafikiwa baada ya taasisi hizo kudaiwa kukumbwa na changamoto ya upungufu wa fedha wakati wa kutekeleza majukumu yake.

Meneja wa TARURA jijini Dodoma mhandisi Goodlucky Mbaga amesema kuwa ongezeko kubwa la uharibifu wa miundombinu ya maji na barabara limekuwa likijitokeza hasa msimu wa mvua hivyo ukarabati unahitajika kwa kiwango kikubwa.

Bw Goodlucky amesema  mkakati uliopo kwa sasa baada ya msimu wa mvua kuisha  ni kuanza na  ujenzi pamoja na uboreshaji wa mifereji  kwenye maeneo yanayopokea maji kutoka sehemu za milima, kwani maji hayo ndiyo huchangia kuharibika kwa miundo mbinu.