Dodoma FM

Rais Dkt.Magufuli aongoza kikao cha kwanza cha Baraza la Mawaziri Ikulu Dodoma

16 December 2020, 2:16 pm

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimkabidhi nyenzo za kazi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein  Mwinyi baada ya kuapishwa kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri  la Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo Desemba 16, 2020

Na,Fred Cheti,

Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli hii leo ameongoza kikao cha kwanza cha Baraza jipya la Mawaziri aliowateua hivi karibuni.
Kikao hicho kimefanyika leo Disemba 16 katika ikulu ya chamwino jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wengine akiwemo Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi na Waziri mkuu Kassim Majaliwa.

Aidha Rais Magufuli amemuapisha Rais mteule wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi ambae pia ni mwenyekiti wa baraza la mapinduzi kuwa Mjumbe mpya wa Baraza la Mawaziri.
Taswira ya habari imezungumza na Mchambuzi wa Masuala ya kisiasa Bw. Michael Kalenge ambae ni Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Mkwawa Iringa juu ya kuanza kazi kwa Baraza hilo ambapo amesema ana imani kubwa litaenda kufanya kazi kwa manufaa ya Watanzania kutokana na aina ya Mawaziri walioteuliwa kuwa na uzoefu .

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akishuhudia Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma akimuapisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo.

Pia Bw.Kalenge amezungumzia suala la baadhi ya mawaziri ambao walikuwepo katika baraza lililopita kuhamishwa wizara ambapo amesema ni jambo zuri kwa kuwa Mh.Rais anatambua uwezo wa kila mmoja.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  akiongoza kikao cha kwanza cha  Baraza la Mawaziri  la Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma leo Desemba 16, 2020

Kwa upande wao baadhi ya wananchi jijini hapa wametoa maoni yao juu ya baraza hilo ambapo wamempongeza Rais kwa uteuzi alioufanya huku wakiamini litakwenda kufanya kazi kwa ajili ya wananchi wote.