Dodoma FM

Watumishi wa wizara ya maji wametakiwa kutekeleza miradi ya maji ipasavyo

8 July 2021, 12:07 pm

Na; Yusuph Hans.

Watumishi katika wizara ya maji wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na nidhani katika matumizi ya fedha na kutekeleza miradi ya maji ipasavyo kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujmla.

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa maji Mh. Jumaa Aweso katika kikao kazi kilichowakutanisha watumishi kutoka kada mbalimbali, ambapo amesema moja ya kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha inapunguza na kumaliza changamoto ya ukosefu wa maji Nchini.

Mh. Aweso amesema kuwa watumishi wa Wizara hiyo hawana budi kujipanga na kuwa na nidhamu katika kazi pamoja na mahusiano mazuri ili kuleta ufanisi katika kazi zao wanazozitekeleza.

Aidha amewataka watumishi hao kuhakikisha wanatafuta wakandarasi wenye uzoefu na weledi katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika na kufanya kazi iliyokusudiwa.

Naye Naibu katibu Mkuu Wizara ya maji Nadhifa Kemikimba amesema kuwa kikao hicho kitasaidia kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji kufuatia kuwepo kwa watumishi kutoka kada mbalimbali ambao watasaidia kuratibu na kupanga shughuli za miradi ya maji.

Katika hatua nyingine Waziri wa maji amesema hatofumbia macho watumishi wote wazembe kazini.