Dodoma FM

Barabara kata ya Mtanana A hadi Ndalibo kuanza marekebisho hivi karibuni

12 May 2021, 1:17 pm

Na; Benald Filbert

Barabara zilizopo katika kata ya Mtanana wilaya ya Kongwa zimeingizwa kwenye bajeti  ya mwaka wa fedha 2021/22  ili kufanyiwa ukarabati kuanzia eneo la Mtanana A hadi Ndalibo, kwa lengo la kuondoa usumbufu ambao wananchi wamekuwa wakikutana nao.

Akizungumza na taswira ya habari diwani wa Kata ya Mtanana Joel Shadrack amesema Kata hiyo imekuwa na barabara korofi hali inayosababisha kukwama kwa  baadhi ya shughuli za maendeleo.

Amesema kupitia bajeti ya Serikali  barabara hizo zitafanyiwa marekebisho ambapo mwezi wa saba zitatangazwa zabuni kwa wakandarasi wenye vigezo vya kufanya kazi hiyo.

Amesema kukamilika kwa barabara hizo katika Kata ya Mtanana itafungua fursa mpya kwa wananchi kuongeza shughuli za ukuzaji wa uchumi.

Barabara nyingi zilikuwa zimeharibiwa na mvua hivyo serikali imekuwa ikijipanga kufanya marekebisho ili kuondoa usumbufu kwa wananchi ikiwepo kukwamisha shughuli za maendeleo.