Dodoma FM

Watu wenye ulemavu watakiwa kujishughulisha na shughuli mbalimbali

5 April 2022, 1:27 pm

Na; Shani Nicolous.                                     

Watu wenye ulemavu wametakiwa kuacha kukaa na kuomba misaada badala yake watafute shughuli za kufanya ili wawezeshwe kufanikisha shughuli zao.

Wito huo umetolewa na Bw. Stephano Nyange Bobo mkazi wa Nzuguni ambaye ni mlemavu wa viungo na anafanya shughuli ya utengennezaji viatu.

Amesema kuwa pamoja na shughuli hizo wanazofanya wanaiomba serikali kuwawezesha kupata mikopo na kuwajengea mazingira rafiki ili waendelee kujitafutia kipato na kuepukana na tabia ya kuombaomba.

Pauleta Lesu ni mke wa Bw. Stephano Nyange Bobo ambaye pia ni mlemavu wa viungo amesema wameamua kujikita katika ujasiriamali na mumewe ili kuepuka kuwa mzigo katika jamii na kutengeneza heshima.

Ameongeza kuwa heshima ya mtu mwenye ulemavu ni kujikubali na kujipambania kuliko kutengeneza dhana ya kudharaulika katika jamii, ameiomba jamii kuacha mawazo mgando na kupuuza vipaji vya watu wenye ulemavu.

Mara kadhaa serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakitoa wito kwa watu wenye ulemavu kufanya shughuli za kujiingizia kipato na kuahidi ushirikiano kwa kuwawezesha mazingira rafiki na mikopo