Dodoma FM

Rais Samia ataka wananchi wasizuiwe kueleza kero zao.

6 April 2021, 9:40 am

Na; Mariam Kasawa.

Rais  wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema viongozi wa kitaifa wakikutana na mabango katika ziara zao, atawaondoa kazini mkurugenzi wa halmashauri na wakuu wa wilaya husika.

Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne  Aprili 6, 2021  Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu aliowateua Aprili 4, 2021.

Amesema imekuwa ni kawaida viongozi wakifanya ziara mikoani na wilayani wanapokewa na mabango ya wananchi wakilalamikia kero mbalimbali na masuala wanayolalamikia si ya kitaifa.

 Amesema wanapokwenda kwenye ziara mikoani  na wilayani wanapokelewa na mabango ya wananchi wakilalamika kero mbalimbali, mabango yale mengine wala siyo mambo au masuala ya kushughulikiwa katika ngazi za juu ni masuala ya kushughulikwa huko chini.

“Kwa hiyo naomba tunapokuja huko mimi na makamu wa rais, waziri mkuu tukikuta bango basi ziwe inshu ya kitaifa lakini siyo mambo ya kushughulikiwa kule chini, nataka niseme  bango moja aidha mkurugenzi au mkuu wa wilaya amekwenda na hii  haina maana mkazuie watu kuandika kero zao,” amesema.

Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Rais Samia ameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi)  kwenda kukusanya mapato na matumizi yafanywe kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo.

Ameitaka Tamisemi kwenda kuongeza usimamizi kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ili kazi ziende vizuri.