Dodoma FM

Siku ya Mtoto wa Kike Duniani, wazazi waaswa kuzingatia malezi

10 October 2024, 10:10 pm

Habiba Mashaka Mohamed toka mkoa wa Katavi akielezea alivyonufaika na kampeni ya Girls Takeover (Msichana Shika Hatmu). Picha na Hilali A. Ruhundwa

Dunia inaadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike huku changamoto zinazomkwamisha mtoto wa kike kufikia ndoto zake hasa katika uongozi zikitafutiwa ufumbuzi kupitia kampeni ya ‘Msichana Shika Hatamu’.

Na Hilali A. Ruhundwa

Wazazi na walezi wameaswa kuhakikisha wanatekeleza jukumu la msingi la kulea watoto kwa kuzingatia usawa wa kinjinsia bila kuathiri mila na desturi. Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Felister Mdemu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyoandaliwa na shirika la Plan International na kufanyikia jijini Dar es Salaam.

Sauti ya Bi. Felister Mdemu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
Mkurugenzi Mkazi wa Plan International Bi. Jane Sembuche akielezea umuhimu wa Siku ya Mtoto wa Kike. Picha na Hilali A. Ruhundwa

Awali Mkurugenzi Mkazi wa Plan International Bi. Jane Sembuche, amesema kuwa wamewezesha wasichana zaidi ya 40 toka sehemu mbalimbali nchini ambao wametumia wiki hii kujifunza uongozi katika ofisi mbalimbali zikiwemo balozi za nchi mbalimbali nchini.

Sauti ya Bi. Jane Sembuche Mkurugenzi Mkazi wa Plan International
Baadhi ya washiriki wa Siku ya Mtoto wa Kike Duniani iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Picha na Hilali A. Ruhundwa

Baadhi ya wasichana walioshiriki kampeni ya Girls Takeover ambao pia wametumia wiki hii kujifunza masuala ya uongozi, wanaelezea waliyojifunza.

Sauti za wasichana wanaoshiriki kampeni ya Girls Takeover

Hata hivyo baadhi ya wadau wameshauri kuwa licha ya kupambania haki za mtoto wa kike, ni vema mtoto wa kiume asiachwe nyuma kwa sababu ndiye baba wa watoto wa kesho. Wametolea mfano wa jinsi amabvyo kwa sasa imekuwa kawaida kwa watoto wa kiume kulelewa na mama watu wazima jambo linaloonekana kuwa hatari kwa siku zijazo.

Sauti ya Bi. Ester Mongi toka Shirika la World Vision akisisitiza mtoto wa kiume kukumbukwa
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania (katikati) akiteta jambo na Mkurugenzi Mkazi wa Plan International (kulia) pamoja na msichana mnufaika wa kampeni ya Girls Takeover. Picha na Hilali A. Ruhundwa

Maadhimisho haya yanajiri ikielezwa kuwa matatizo ndani ya familia yanachangia kwa kiasi kikubwa matunzo mabaya kwa watoto ambapo asilimia 22 ya wasichana wenye umri wa miaka 15-19 walipata ujauzito kwa mwaka 2022 huku mikoa vinara wa ndoa za utotoni ikiwa ni Songwe, Ruvuma, Katavi, Rukwa na Mara.

Kila mwaka tarehe 11 Oktoba, Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Kike ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Msichana na uongozi, tumshirikishe wakati ni sasa’.