TADB yaongeza kiwango kikubwa utoaji wa mikopo sekta ya kilimo
30 July 2026, 17:06

Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi za kifedha kuhakikisha sekta ya kilimo inapata mtaji wa kutosha ili kuongeza uzalishaji, kuimarisha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imesema imeongeza kwa kiwango kikubwa utoaji wa mikopo kwa sekta ya kilimo, ambapo katika kipindi cha miaka minne tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani mwaka 2021, benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 1.55 kwa wakulima nchini.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Amesema kuwa wakati Rais Samia alipoingia madarakani, jumla ya mikopo yote iliyokuwa imetolewa na benki hiyo ilikuwa takribani shilingi bilioni 294 pekee, lakini hadi sasa kiwango hicho kimeongezeka maradufu na kufikia shilingi trilioni 1.55.
Ameongeza kuwa benki hiyo imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wakulima wadogo kupitia dirisha maalumu la mikopo, linalowalenga wakulima wasiokuwa na uwezo wa kukidhi masharti ya mikopo ya kawaida, hatua inayolenga kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji wa kilimo.
Aidha, Nyabundege amesema mafanikio ya uwekezaji katika sekta ya kilimo yamechangia kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini, ambapo uzalishaji umefikia tani milioni 22.8 mwaka 2025, kiwango kinachoonesha kuwa Tanzania inaendelea kuwa na utoshelevu wa chakula.